Miaka ya hapo katikati kutokana na kutekwa na utamaduni wa Kimagharibi, Watanzania walijikuta wakidharau kutumia dawa za asili na kutukuza zile za kigeni.
Pia dawa hizi zilionekana ni kwa ajili ya kundi la watu fulani (maskini), kwani wengine wakiugua wanapanda ndege kwenda kutibiwa nje au hata kama ni hapa nchini basi kwenye hospitali binafsi zinazotoza fedha nyingi.
Lakini kadiri miaka inavyozidi kwenda, kwa sasa watu wamezinduka na kuanza taratibu kurudia tiba asili ukizingatia kwamba pia kumekuwepo na magonjwa mengi yanayoibuka na kukuta yakikosa tiba hospitalini.
Kama vile haitoshi magonjwa mengi yanayosumbua watu, ikiwemo saratani, shinikizo la damu yanaelezwa kwa asilimia kubwa yanatokana na mfumo wa maisha yetu ikiwemo vyakula tunavyokula.
Hivyo basi unapokwenda kwa wataalamu wa matatizo kama haya, utakuta unaambiwa ule vyakula vya asili, na hapo ndipo watu wanapojikuta pia wakirudi kwenye dawa za asili.
Suala hili pia limetokana na ukweli kwamba kuna baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakitumia dawa za kisasa hadi kuwa sumu mwilini mwao na pale wanapoamua kurudi kwenye dawa asili tayari figo zinakuwa zimechoka.
Hivi karibuni nilifanikiwa kukutana na mganga wa tiba asili na mbadala, Abdallah Mandai ambaye ana kituo chake maeneo ya Mongo la Ndege, jijini Dar es Salaam kinachofanana kabisa na hospitali za kisasa katika utoaji huduma zake.
Katika mahojiano hayo nilitaka kujua ni namna gani ameweza kufanikiwa na kufika hapo na changamoto anazoziona katika aina hiyo ya tiba.
Mandai anaanza kwa kusema kwamba anashukuru kwa sasa watu kuanza kuamini dawa zao tofauti na hapo awali.
Kutokana na hali hii mganga huyu amewataka matabibu wenzake kubadilisha utaratibu wa utoaji matibabu ili wananchi waendelee kujenga imani nao.
“Unajua kutokana na namna baadhi ya waganga wenzetu ambavyo wamekuwa wakifanya shughuli hizi, mfano katika mazingira machafu, kutumia tunguli, kuwa na muonekano mbaya, kulifanya watu kutoamini tiba zetu hata kama mganga husika dawa zake zitakuwa zinatibu.
“Ni kwa kuligundua hilo mimi nilibahatika kutembea baadhi ya nchi kama Afrika Kusini na kujifunza namna ambavyo wamekuwa wakifanya shughuli hii, na nilipambana nikaaingia hadi darasani kwa muda wa miezi mitatu.
“Hivyo baada ya kurudi hapa nchini nikaona kuna haja ya kuleta mabadiliko na ndipo hapo nilipofungua kituo kidogo cha kutoa matibabu ambacho kilikaribia kufanana na zahanati.
“Hata hivyo kutokana na uwingi wa watu niliamua kununua tena sehemu eneo la jirani na kujenga kituo kikubwa ambacho hiki sasa kimegawanyika, ikiwemo sehemu ya kupimia, ya kumuona daktari, ya kutoa dawa, mapokezi, sehemu ya kukaa wagonjwa na ya kupumzisha wagonjwa wanaokuja wakiwa katika hali mbaya,” anasema.
Aidha ndani ya kituo hicho anasema kuna mashine maalumu kwa ajili ya wagonjwa waliopooza na wale wanaotakiwa kushtuliwa mishipa ya fahamu kwani huwa anapokea wagonjwa wa aina mbalimbali.
“Hatua hii ndiyo imenifanya nipate wateja wengi ikiwemo maarufu na wanaoheshimika katika jamii na hii kwa kuona kwamba hata akifika kwangu mchana hakuna atakayemshangaa kwa kuwa kumekaa kihospitali kabisa,” anasema.
Ili kupata matibabu yaliyo sahihi, Mandai anasema abadani hampatii mgonjwa dawa bila ya kumpima ili kuepuka kumpa tiba isiyo halali yake.
Wito wake kwa waganga wengine ni kusoma zaidi vitabu vya tiba mbadala ili kuweza kuendana na mahitaji ya sasa kwa kuwa shughuli za tiba kila siku zinaenda zikibadilika.
Wakati kwa upande wa serikali aliishauri kuangalia utaratibu wa kufungua shule ya tiba mbadala ili kuweza kurithisha elimu hiyo na kwa vizazi vijavyo na kuachana na ule mtindo wa kurithi kifikra kutoka kwa wazazi.
Kama vile haitoshi, anataka kuwepo na sheria itakayoruhusu kubadilishana wagonjwa kutoka tiba mbadala na kwenda tiba ya kisasa, ambako mgonjwa anaweza kupewa rufaa pale ugonjwa wake unaposhindikana kutibika upande mmoja wa tiba.
Mandai anaenda mbali zaidi na kutaka kutengwa kwa maeneo maalumu ya miti dawa kama inavyofanywa kwa hifadhi za jamii, ili wanaofanya shughuli hizo iwe rahisi kupata dawa kwa kuwa ukweli ni kwamba wengine wanalazimika kuziagiza kutoka nchi jirani wakati hapa nchini kuna misitu ya kutosha.
“Kwa kufanya hivi hata sasa wenye kufanya shughuli hizi tutakuwa wepesi kubeba jukumu la kuhifadhi misitu hiyo kwa kuwa tunajua ndiyo vyanzo vyetu vya kupatia dawa,” anasema.
Pia kwa wananchi aliwataka kuhakikisha wanatunza vyanzo vya miti kwa kutoharibu mazingira, kwani hii itawezesha kuwapunguzia gharama za kupata matibabu katika hospitali ambako wengi wao wameonekana kushindwa au kupoteza wapendwa wao kutokana na kukosa fedha.
Source:
Nasra Abdallah