Anzisheni mashamba ya Dawa Asilia - BAWATA

Baraza la Waganga Watafiti na Tiba Asilia Tanzania (BAWATA), limetoa mwito kwa wataalam wa fani ya tiba asilia kuanzisha mashamba yatakayopandwa mimea inayotumika kama dawa asilia ili kuilinda isipotee.

Wito huo umetolewa juzi na Mwenyekiti wa BAWATA, Tabibu Mohamed, kwa wachimba mawadawa, wauza madawa, waganga wa tiba asilia na wakunga wa jadi.

Mohamed alisema mimea ya dawa inaweza kupotea kutokana na mabadiliko ya tabia nchi inayosababisha ukame na tatizo la ukataji wa miti katika misitu hivyo husababisha kupotea kwa mimea mingi inayotumika kama mitidawa ama tiba asilia.

Kutokana na hali hiyo, Mohamed aliwataka waamke na kuacha kutegemea kuvuna mitidawa iliyokuwepo tangu enzi na enzi kwa kuwa imeanza kutoweka kwa kasi ya ajabu.

“Ni vyema wataalam wote wa fani ya tiba asilia wakaanzisha mashamba na kuvitunza vyanzo vya mito na chemchem za maji huku wakizuia wananchi kulima ama kukata miti hovyo kwenye maeneo hayo ili kutunza uoto wa asili” alisema.

Katika hatua nyingine, Bodi ya BAWATA imemteua Dk. Khalid Shariff King kuwa Katibu Mkuu wa baraza hilo.

Source:

na Janet Josiah


© 2025 Shirika la Maendeleo Utafiti na Tiba Tanzania - SHIMAUTITA